Online

Tuesday, May 3, 2016

EPL News: David De Gea bora zaidi Manchester United kwa mara ya tatu mfululizo

Mlinda mlango wa Manchester United David de Gea ametajwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Manchester United
MLINDA mlango wa Manchester United David De Gea ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka ya Sir Matt Busby kwa mara ya tatu mfululizo.
De Gea alipata kura nyingi zilizopigwa na wajumbe wa klabu hiyo ya Old Trafford wakati wa tuzo za Mchezaji Bora wa Mwaka, na Muhispania huyo amefuata nyayo za Cristiano Ronaldo kwa kushinda tuzo hiyo mara tatu, lakini Ronaldo hakutwaa tuzo hiyo miaka mitatu mfululizo, hivyo kumfanya De Gea kupigia mstari hadhi yake kama mchezaji mahiri katika msimu huu.
Mlinda mlango huyo wa Uhispania mwenye umri wa miaka 25, aliokoa michomo ya hatari itakayoendelea kukumbukwa dhidi ya Southampton, Watford na hivi karibuni kabisa katika nusu-fainali za Kombe la FA dhidi ya Everton.
Chris Smalling (kulia) akiwa sanjari na Wayne Rooney baada ya kupokea tuzo yake
“Kila mmoja anafahamu kwamba alialikwa kucheza Real Madrid,” alisema van Gaal.
“Mpenzi wake anaishi katika Real Madrid, wazazi wake ni Wahispania, na Real Madrid ni klabu kubwa, lakini bado yupo hapa, nami kama meneja nafurahia kuwa naye hapa na amestahili kutwaa tuzo hii.”
Marcus Rashford na Cameron Borthwick-Jackson, ambao walivumbuliwa kutoka timu ndogo Fletche Moss, walitwaa tuzo za Mchezaji Bora wa Umri chini ya miaka 18 na 21.
“Limekuwa jambo la kipekee, ni vigumu kujikubali,” Rashford alieleza katika mahojiano yake na televisheni.
Marcus Rashford akiwa na tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi sanjari na kocha mkuu wa Akademi Nicky Butt
 “Nimepata upendeleo (kuitwa kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya Midtjylland), kwa sababu nilikuwa nikifikiria sana kuhusu kucheza, kwa hiyo sikuwa na sababu ya kufikiria tena.
“Ina maana kubwa sana. Mimi ni mzawa wa Manchester. Ni ndoto yangu iliyoanza kutimia.”
Borthwick-Jackson aliongeza: “Ni heshima kubwa kwangu, kutwaa tuzo hii, inajenga ndoto zangu.”
 “Nimefanikiwa kuwa juu katika kila rika, kwa hiyo ni ndoto yangu.
“Sina hofu, najua ni ngumu kusema, lakini huwa napenda kutoangalia umati wa watu ili nicheze. Natambua nalipwa kwa ajili ya michezo.”
Naye fowadi wa Ufaransa, Anthony Martial alitwaa tuzo ya Bao Bora la Msimu kwa bao lake la juhudi binafsi dhidi ya Liverpool Septemba, 2015, akimshinda Rashford na bao lake dhidi ya Manchester City na West Ham, hali kadhalika bao lake mwenyewe dhidi ya Stoke.
Mlinzi Chris Smalling ametwaa tuzo ya Mchezaji wa Mwaka pia.
“Ni heshima kubwa kupata tuzo hii, kama nilivyopigiwa kura na wachezaji,” alisema Smalling. “Majina makubwa yametwaa tuzo hii, hivyo jina langu linaongezeka kwenye orodha ya wakuu hao.”

TUZO ZILIZOTOLEWA NA MANCHESTER UNITED KWA WACHEZAJI WAKE 
Mchezaji Bora wa Mwaka: David de Gea
Mchezaji Bora wa Wachezaji: Chris Smalling 
Mchezaji Bora Kinda wa Mwaka chini ya 21r: Cameron Borthwick-Jackson 
Mchezaji Bora Kinda wa Mwaka chini ya 18: Marcus Rashford 
Bao Bora la Msimu: Anthony Martial v Liverpool  

EPL News: Ranieri ampigia siku Hiddink kumshukuru kwa tajiAKIWA mwingi wa furaha, meneja wa Leicester City, Claudio Ranieri alimpigia simu bosi wa Chelsea Guus Hiddink baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Tottenham Hotspur Jumatatu usiku, mchezo uliowapa ubingwa Leicester City.
Ranieri, 64 alikuwa meneja wa Chelsea baina ya mwaka 2000 - 2004 na alikuwa kipenzi cha mashabiki katika Stamford Bridge licha ya kutoshinda mataji.
Nafasi yake ilichukuliwa na Jose Mourinho mwaka 2004, lakini aliendelea kubaki kwenye mioyo ya mashabiki wa Chelsea tangu hapo. Muitaliano huyo ni mcheshi, babu mfano wa kuigwa na wengi na mmoja wa mashabiki wa Chelsea alionyesha ishara akisema: “Fanya Ranieri” na mashabiki wa Chelsea waliimba jina lake na “Leicester, Bingwa!” baada ya kipyenga cha mwisho dhidi ya Tottenham.
Chelsea kwa kuilazimisha Tottenham sare ya mabao 2-2 wamempatia Ranieri ubingwa baada ya Eden Hazard kufunga bao la kusawazisha dakika za majeruhi. Kocha huyo wa zamani wa Chelsea alipaa kwenda nchini Italia Jumatatu kumsalimu mama yake mwenye umri wa miaka 96 na atakaporejea England atapokelewa kama shujaa huku timu yake ikiweka historia naye pia hali kadhalika.

Haya ndiyo aliyosema Hiddink akizungumzia simu ya Ranieri. “Baada tu ya kipyenga cha mwisho, dakika chache baada ya judo, nilipokea simu kutoka kwa Ranieri. Alitushukuru hasa kwa kile tulichofanya kipindi cha pili na nilimpongeza kwa kutwaa ubingwa.
Wamestahili, inashangaza na huenda hata ikaleta mshtuko kwa klabu iliyopambana hadi mwisho.
“Sikuona machozi yoyote kwa sababu tulikuwa tukizungumza kwenye simu lakini sauti yake iliashiria alikuwa akitetemeka kidogo. Alisema asante mara tano.”

VPL: Stand United v Yanga SC: Stand kuisimamisha Yanga?

Yanga ikiichapa Stand itakuwa na uhakika wa 100% kutwaa taji la VPL 2015-16
Vinara wa Ligi ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga leo watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujiweka karibu na ubingwa endapo wataifunga Stand United kwenye mchezo wa ligi hiyo utakayopigwa uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Yanga yenye pointi 65, italazimika kushinda mchezo huo ili kujihakikishia taji hilo ambalo hadi sasa ina asilimia 95 yakulichukua kwa mara ya pili baada ya kuongoza kwa tofauti ya pointi sita kati yake na Azam FC, inayoshika nafasi ya pili huku ikiwa imebakiwa na michezo minne kabla ya msimu kumalizika.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0, hivyo wenyeji Stand wataingia katika mchezo huo wakiwa na kazi ya kuhakikisha wanalipa kisasi cha kupoteza mchezo wa kwanza lakini swali kubwa kwao, ni, je wataweza kuizuia safu ya ushambuliaji ya Yanga isifunge bao.
Stand wanaingia kwenye mchezo huo wakitoka kufungwa mabao 2-1 na ndugu zao Mwadui FC, kwenye mchezo uliopita matokeo ambayo yamemkasirisha kocha wake Mfaransa Patrick Liewig, hivyo ni wazi atataka kupambana ili waweze kushinda mchezo huo ili waweze kumaliza msimu kwenye nafasi za juu.
Ingawa pointi 34, walizo nazo Stand zimewaweka sehemu salama lakini bado mchezo huo hauwezi kuwa mwepesi kwa Yanga , kutokana na kikosi cha Stand kuundwa na nyota wengi waliowahi kuzichezea timu kubwa nchini za Simba na Yanga.
Kocha wa Stand United  Liewig, amesema amekiandaa vizuri kikosi chake kwa ajili ya kushinda mchezo huo ambao utawasaidia kumaliza msimu kwenye nafasi nzuri zaidi kuliko waliyo sasa.
Liewig amesema anajua anakwenda kupambana na timu ngumu inayoongoza ligi lakini wamejipanga kuhakikisha wanacheza vizuri na kushinda kutokana na maandalizi waliyoyafanya mara baada ya kumalizika mchezo wao uliopita dhidi ya Mwadui FC.
“Najua Yanga ni timu nzuri na bora kwa sasa Tanzania lakini kama Stand tumejipanga kuhakikisha hatuwi ngazi ya wao kutangaza ubingwa kwetu tutajitahidi kupambana ili kupata ushindi kwenye uwanja wa nyumbani lengo ni Stand kumaliza kwenye nafasi za juu tofatu na tuliyopo hivisasa,” aliesema Liewig.
Katika mchezo huo kocha Liewig, atakuwa akiwategemea zaidi wachezaji wake Elias Maguli, kiungo Amri Kiemba na Haruna Changongo ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi chake huku safu ya ulinzi ikiwa chini ya Nassor Masouc ‘Chollo’ , Abuu Ubwa na Rajabu Zahiri.
Kwa upande wa kocha wa Yanga Hans van der Pluijm, amesema amekwenda Shinyanga kwa ajili ya pointi tatu na ana uhakika wa kuzipata kutokana na uimara wa kikosi chake ambacho kimekuwa kikiimarika katika kila mechi wanayo cheza hivi sasa.
Pluijm amesema anaiheshimu Stand United kuwa ni moja ya timu nzuri na ngumu ambayo inaundwa na wachezaji wengi wazoefu lakini  anajivunia ubora wa wachezaji wake ambao ushiriki wao katika michuano ya kimataifa umewapa uzofu mkubwa na ndiyo sababu ya matokeo ya ushindi wanao upata
“Hizi ni mechi muhimu hivyo tusingependa kuzifanyia mzaha kwasababu tunataka ubingwa na kila mchezaji ndani ya timu analijua hilo llengo letu ni kuhakikisha tunachukua pointi tatu nyingine hapa ili twende kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho tukiwa na rekodi nzuri ya ushindi kwenye mechi za ligi,” alisema Pluijm
Pluijm amesema kikosi chake cha leo hakitakuwa na mabadiliko makubwa sana tofauti na kile kilichoanza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Toto Africans, ambapo katika safu ya ushambuliaji akiendelea kuwatumia mapacha wawili Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao wote kwa pamoja wamefunga mabao 33 huku kwenye kiungo akiwaanzisha Haruna Niyonzima na Mzimbabwe Thabani Kamusoko.

Monday, May 2, 2016

UEFA: Bayern Munich v Atletico Madrid: Bayern kufuta mzimu wa kuondolewa na timu za Uhispania

Bayern Munich v Atletico Madrid
BAYERN MUNICH ina kazi kubwa kulipa deni la kipigo cha bao 1-0 watakapoikaribisha Atletico Madrid kwenye mchezo wa marudiano ya nusu-fainali ya Champions League utakaopigwa uwanja wa Allianz Arena, mjini Berlin, Ujerumani Jumanne usiku.
Vinara hao wa Bundesliga wanacheza nusu-fainali ya Champions League kwa mara ya tano mfululizo huku wakifanikiwa kutinga fainali mara mbili msimu wa 2011-12 ambapo walifungwa na Chelsea na 2012-13 walipoifunga Borussia Dortmund. Na katika nusu-fainali mbili za mwisho timu hiyo ilitolewa na timu za Uhispania.

Walipoteza kwa Real Madrid msimu wa 2013-14 kisha wakaangukia pua mbele ya Barcelona kwenye msimu wa 2014-15. Sasa watakuwa wakijitahidi kuepuka kutolewa na wapinzani wengine kutoka Uhispania mfululizo.
Washindi wa pili wa michuano hiyo msimu wa 2013-14, Atletico Madrid wanacheza kwa mara ya tatu hatua ya nusu-fainali ndani ya misimu mitatu na wanapewa nafasi ya kuwafunga wapinzani wao kutoka Ujerumani. Shukrani kwa bao la Saul Niguez ambalo liliwapa vijana wa Diego Simeone ushindi mwembamba kabla ya kikipiga Ujerumani Jumanne.
Kiwango cha timu zote
Bayern Munich wameshinda mechi 7, sare 2 na kufungwa 2 katika mechi 11 za Champions League msimu huu. Wamekuwa na wakati mgumu katika mechi za ugenini, lakini uwezo wao wa kugawa dozi nzito wawapo nyumbani umewasaidia kuendelea kudumu katika michuano hii.
Rekodi ya Atletico Madrid kwenye Champions League msimu huu pia inaeleweka; ushindi 7, sare 2 na imefungwa mara mbili pia katika mechi 11 huku wakicheza mechi 7 bila kuruhusu bao.
Jerome Boateng alicheza dakika 68 Bayern Munich ikipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Gladbach wikiendi iliyopita na kuna uwezekano mkubwa akaanza kwenye mchezo dhidi ya Atletico huku Mehdi Benatia akicheza kama mlinzi wa kati.
Arjen Roben na Holger Badstuber bado wanaendelea kubaki majeruhi wakati Sebastian Rode bado hakijaeleweka kwani anaugua.

Bayern Munich: Kikosi kinachotazamiwa (4-1-4-1)

Neuer, Bernat, Benatia, Boateng, Lahm, Alonso, Muller, Vidal, Thiago, Costa, Lewandowski.

Atletico Madrid: Kikosi tarajiwa (4-4-2)

Oblak, Felipe Luis, Savic, Godin, Juanfran, Koke, Fernandez, Gabi, Saul, Torres, Griezmann.

La Liga News: Nataka Zidane aendelee kuwa kocha Madrid - Ronaldo

Wachezaji wa Real Madrid wanafurahia uwepo wa Zinedine Zidane
Nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo amefungua yaliyo moyoni mwake baada ya kudai kuwa anapenda kumuona Zinedine Zidane akiendelea kuinoa timu hiyo msimu ujao.
Zidane - nyota wa zamani wa Juventus na Ufaransa, alikabidhiwa kibarua cha kuinoa Madrid Januari akichukua nafasi ya Rafa Benitez, baada ya kufanya kazi kama kocha msaidizi chini ya Carlo Ancelotti na akiwa kama meneja wa Real Madrid Castilla.
Real Madrid imeshinda mechi 18 kati ya 23 tangu Zidane aingie madarakani na kuiwezesha timu hiyo kurejea kwenye mbio za ubingwa La Liga huku ikitinga nusu-fainali Ligi ya Champions League.
Ronaldo ambaye anatarajia kuwa fiti kwa mechi ya marudiano dhidi ya Manchester City Jumatano ijayo, ameiambia tovuti ya klabu hiyo jinsi wachezaji wanavyojisikia kukubalika zaidi chini ya Zidane.
“Nadhani tunahisi kuwa na furaha zaidi chini ya Zidane. Tunahisi upendo wake, tunajua kwamba yupo katika kipindi cha kuzoea mazingira, lakini mambo yamemnyookea kwa haraka sana nami namfurahia pia,” alisema nahodha huyo wa Ureno.
Cristiano Ronaldo katika mazoezi kujiandaa na mchezo wa nusu-fainali ya Champions League dhidi ya Manchester City Jumatano ijayo
“Daima nilivutiwa naye kama mchezaji, na sasa ni kocha hali kadhalika, jinsi anavyofanya mambo yake na kushughulika na wachezaji. Jinsi anavyofundisha tu ningependa aendelee kubaki Real Madrid.”
Zinedine Zidane ameshinda mechi 10 mfululizo kwenye La Liga huku akizitia presha Barcelona na Atletico Mdrid zinazoongoza msimamo wa Ligi.
Ili wapate ubingwa ambao hawapewi nafasi kubwa kuutwaa ni sharti wapinzani wao wapoteze mechi au kutoa sare kati ya sasa na mwisho wa msimu..
Wakati huo pia wana kibarua kingine cha kuikabili Manchester City katika mechi ya marudiano nusu-fainali Champions League utakaopigwa Santiago Bernabeu Jumatano ijayo.
 
Copyright © 2011. The Chief - All Rights Reserved.