Online

Friday, September 16, 2011

Bodi ya Korosho Tanzania yatangaza bei dira ya korosho kwa msimu wa 2011/12

Lindi

Bodi ya korosho Tanzania chini ya mwenyekiti mpya Bi Anna Abdallah, jana imetangaza bei dira ya zao la korosho nchini kwa msimu wa mwaka 2011/12.

Akiongea na Pride fm katika kipindi cha Amka na Pride kwa njia ya simu kutoka mkoani Lindi, mwandishi wa habari wa gazeti la serikali Habari Leo, Hassan Simba amesema kuwa, katika mkutano huo wa wakulima na wadau wa zao la korosho ulioanza juzi na kufikia tamati jana katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Oceanic uliopo mjini Lindi, bei hiyo ni kwa nchi nzima.

Aidha Simba amesema kuwa katika mkutano huo wa jana, uligubikwa na kutooelewana baina ya wakulima na wawakilishi wao baada ya kutaka kubadilishiwa ajenda ya mkutano.

Awali ilifahamika kwamba wakulima hao na wadau wengine wangejadili ajenda ambazo hazikuweza kujadiliwa katika kikao cha mjini Dodoma hivyo kuwafanya wakulima na wadau hao kujiandaa kwazo. Lakini mara tu baada ya kuanza kwa mkutano huo wakulima hao walibadilishiwa ajenda na kuambiwa wasingeweza kujadili ajenda zaidi ya moja ambayo ilikuwa inahusu bei dira ya zao la korosho, jambo lililosababisha kutoelewana.

Kutokana na kutoelewana huko ambako ilionesha wazi kungepelekea kuvunjika kwa mkutano huo, ndipo zikatumika busara za mwenyekiti wa Bodi ya Korosho na kunusuru mambo.

Katika mkutano huo, ndipo ilipotangazwa bei dira hiyo kwa msimu wa 2011/12 ambapo korosho ghafi daraja la kwanza itauzwa Shilingi 1,200 na daraja la pili Shilingi 960 kwa kilo.

Bei ya 1,200, imekuja baada ya kuwepo mjadala juu ya bei stahili kwa zao hilo msimu huu ambapo hoja iliyowekwa mezani kujadiliwa ilikuwa ni Shilingi 939 kwa kilo moja, lakini baada ya majadiliano ndipo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu akapendekeza Shilingi 1,200 kwa kilo moja, hoja iliyokubaliwa na wajumbe.

Aidha kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano wa Bodi ya Korosho Tanzania, bei hiyo inatokana na utafiti uliofanywa katika soko la Korosho la Dunia nchini India na kulinganisha thamani ya fedha ya Tanzania, India na Dola ya Marekani..

Chanzo; Pride fm

No comments :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. The Chief - All Rights Reserved.