Online

Wednesday, December 28, 2016

VPL: Yanga SC v Ndanda FC: Ngoma arejea, tayari kuiangamiza Ndanda leo Uhuru

KOCHA Mkuu George Lwandamina na kikosi chake cha Yanga SC leo Jumatano watakuwa na nafasi nyingine ya kurekebisha makosa yao na kupunguza pengo la pointi kati yao na Simba SC, itakapowaalika Ndanda FC kutoka mjini Mtwara katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utakaopigwa uwanja wa wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani wa aina yake, kwa sababu licha ya kuwa wenyeji, lakini Yanga wanalazimika kupambana ili kupata ushindi wakifahamu kuwa Ndanda ni moja ya timu ambayo inawasumbua sana bila kujali wanacheza nyumbani au ugenini.
Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kulazimishwa sare ya bao 1-1 na African Lyon katika mchezo ambao ulipigwa uwanja wa Uhuru pia, hivyo matokeo hayo kuwafanya kuwa nyuma ya vinara wa ligi hiyo Simba SC kwa pointi nne.
Nayo Ndanda chini ya kocha Selemani Matola, hawana matokeo mazuri tangu kuanza kwa mzunguko wa pili. Imepoteza mechi zote mbili ilizocheza nyumbani - ilichapwa mabao 2-0 na Simba kisha ikachapwa idadi kama hiyo na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Nangwada Sijaona mjini Mtwara - matokeo ambayo yanawafanya wawe na morari wa kupambana.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa katika dimba la Nagwanda Sijaona mjini Mtwara, timu hizo zilitoka sare ya 0-0, hivyo kila upande kuwa na nia moja tu ya kuibuka na ushindi katika mchezo wa leo.
Kufuatia sare dhidi ya African Lyon, ni wazi kuwa Yanga wataingia kwa nia ya kutaka pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo wakitumia mbinu ya kulishambulia sana lango la wapinzani wao ili kupata mabao ya mapema yatakayo wahakikishia ushindi.
Kuelekea mchezo huo, Yanga itamkaribisha mshambuliaji wake Mzimbabwe Donald Ngoma, ambaye aliukosa mchezo uliopita kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za manjano, na anatarajia kuanzishwa kikosi cha kwanza sanjari na Amissi Tambwe ambaye alifunga bao la kusawazisha kwenye mchezo uliopita.
Licha ya kurejea kwa Ngoma, lakini kumeonekana kuwa na hali ya utulivu kwenye kikosi cha Yanga baada ya kumalizika kwa mgomo wa wachezaji ambao ulisababisha timu kushindwa kufanya mazoezi, kwa siku mbili na kupelekea matokeo ya sare.
Tayari uongozi wa timu hiyo umemaliza kesi hiyo kwa kulipa mishahara na posho zote walizokuwa wakidai wachezaji.
Mfumo ambao umekuwa unatumiwa na kocha Lwandamina ni 4-3-3, ambapo mshambuliaji mpya wa timu hiyo Emmaneuli Martin, naye anatarajiwa kupewa dakika nyingi za kucheza kwenye mechi ya leo baada ya kuonesha kiwango kizuri kwenye mechi iliyopita.
Tegemeo kubwa la Ndanda katika safu ya ushambuliaji ni Omary Mponda na Riphat Hamisi ambao wamesafiri na kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya pambano hilo gumu.
Kocha Matola, atakuwa anahitaji kuwapoza mashabiki wa Ndanda baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo.

No comments :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. The Chief - All Rights Reserved.