Online

Sunday, January 1, 2017

EPL: Premier League round-up: Chelsea haikamatiki, Liverpool yaibamiza Manchester City, United, Burnley, Bournemouth zashinda

VINARA Chelsea waliendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Premier League wakiendeleza ushindi katika kulisaka taji hilo. Sasa wakishinda mara 13 katika mechi 13 wakiibamiza Stoke City mabao 4-2 wakati Liverpool wakijikita katika nafasi ya pili baada ya kuichapa Manchester City bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Anfield.
Liverpool iliichapa Manchester City bao 1-0 kumaliza mwaka 2016. Georginio Wijnaldum akifunga bao pekee.

Hii hapa ni round-up ya mechi 7 zilizopigwa Jumamosi Disemba 31, 2016 ikiwa ni mechi za kufungia mwaka.
 
Chelsea 4-2 Stoke City
Chelsea ilijihakikishia ushindi wa 13 mfululizo kwenye ligi na kuongeza pointi wakijichimbia zaidi kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Mabao mawili ya Willian na mengine kutoka kwa mlinzi Gary Cahill na mshambuliaji Diego Costa yaliisaidia the Blues kulisogelea taji hilo mbele ya Liverpool iliyokuwa na kibarua kigumu dhidi ya Manchester City.
Stoke ilisawazisha mara mbili tofauti kupitia kwa Bruno Martins Indi na Peter Crouch.
Vijana wa Antonio Conte watasafiri kwenda White Hart Lane Jumatano usiku wakijua kuwa ushindi pekee utawafanya kuifikia rekodi ya Arsenal kushinda mechi 14 mfululizo kwenye ligi.
Kichapo kinamfanya Mark Hughes na Potters kutokuwa na ushindi kwenye mechi tano za ligi.
Manchester United 2-1 Middlesbrough
Manchester United ilirekodi ushindi wakitoka nyuma kwa bao 1-0 na kuichapa Middlesbrough mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Old Trafford.
Grant Leadbitter aliwafungia vijana wa Aitor Karanka bao la kuongoza, lakini mabao mawili katika dakika tano za mwisho kutoka kwa Anthony Martial na Paul Pogba yaliwahakikishia the Red Devils ushindi wa tano mfululizo mwezi Disemba.
Ushindi unamfanya Jose Mourinho kulingana pointi na Tottenham.
Leicester City 1-0 West Ham United
Leicester ilipata ushindi wa pili kwenye ligi kwenye mechi 10 wakiichapa West Ham bao 1-0 katika mchezo uliopigwa King Power Stadium.
Islam Slimani alifunga kwa kichwa na kuisaidia timu ya Claudio Ranieri kupaa kwa pointi sita kutoka eneo la kushuka daraja.
Kichapo kinamaanisha mwisho wa ushindi mara tatu mfululizo kwa Hammers, ambao wanaangukia nafasi ya 13 kwenye msimamo.
Burnley 4-1 Sunderland
Burnley iliendeleza kiwango kizuri katika uwanja wa nyumbani wakiichapa Sunderland mabao 4-1 wakirekodi ushindi wa saba katika mechi 11 katika dimba la Turf Moor.
Andre Gray alifunga hat-trick na Ashley Barnes akafunga kwa mkwaju wa penalti kuihakikishia timu ya Sean Dyche kupaa hadi nafasi ya 11 kwenye msimamo. Jermain Defoe akafunga bao la kufutia machozi kwa wageni, lakini halikusaidia chochote.
Matokeo yanamfanya David Moyes kuwa pointi mbili chini ya mstari salama.
Southampton 1-2 West Bromwich Albion
West Brom iliendelea kuwa na msimu mzuri wakitoka nyuma na kuichapa Southampton mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa St Mary’s.
Shane Long aliwapa Saints bao la kuongoza, lakini Matt Phillips alisawazisha na bao la Hal Robson-Kanu likaihakikishia Baggies kuondoka South Coast kwa ushindi.
Matokeo hayo yanaifanya timu ya Tony Pulis kupata nafasi ya nane wakitokea nafasi ya tisa.
Swansea City 0-3 AFC Bournemouth
Bournemouth ilipata ushindi wa pili ugenini msimu huu wakiichapa Swansea ambayo haina meneja kwa mabao 3-0.
Mabao ya Benik Afobe, Ryan Fraser na Josh King yaliihakikishia ushindi Cherries dhidi ya timu dhaifu ambao inaongozwa na meneja wa muda Alan Curtis.
Kwa matokeo hayo Swansea wanazidi kujichimbia mkiani mwa msimamo kuelekea Mwaka Mpya.

No comments :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. The Chief - All Rights Reserved.