Online

Monday, May 22, 2017

Marafiki wa NDANDA F.C 3-0 Wanafiki wa NDANDA F.C


HAKUNA kitu kizuri kama kushinda vita – kumshinda adui yako ni moja kati ya vitu vinavyofurahisha nafsi katika hali ya upeo wa juu sana. Unapomshinda adui yako unamaanisha ushujaa wako katika kila hali. Unakuwa umemshinda kwenye mbinu za kupigana. Kama haitoshi, unakuwa umemshinda kwenye namna ya uwezo wa kupambana.
Kwa hivi pia unakuwa umemdhalilisha – na hakuna kitu ambacho wengi hawakipendi kama kudhalilishwa. Watu walioshindwa vita hushindwa kila kitu; hujiona wako chini na hawawezi hata kuinua sauti mbele yako. Hujiona wamekuwa dhaifu mbele yako kwa sababu kwanza umempiga lakini pia umejua udhaifu wake.

Kwa namna hii ndivyo ilivyokuwa kwa marafiki wa Ndanda FC ambao wakati huu wanafurahia ushindi wao wa 3-0 dhidi ya wanafiki wa Ndanda FC. Hakuna kitu kinachowafurahisha kama kuwaziba midomo wanafiki – hili ndilo bao la kwanza. Wapo waliokuwa wanaomba kila siku Ndanda FC ishuke daraja kwa sababu wanazozijua wao wenyewe. Ndanda FC kusalia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ni ushindi mkubwa kwa marafiki wa Ndanda.
Bao la pili kwa marafiki wa Ndanda dhidi ya wanafiki wa Ndanda linakuja pale ambapo wengi walidhani kutokana na ukata mkubwa uliowasumbua kwa muda mrefu timu hiyo ingeshindwa kufurukuta katika kumalizia duru la pili Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ni katika kipindi ambacho kila mtu alikuwa anaisubiri May 20 kuthibitisha kuwa Ndanda FC imerudi rasmi Ligi Daraja la Kwanza.

Bao la tatu wanafiki wa Ndanda wamefungwa pale walipojisahau wakidhani kuwa Ndanda FC ilikuwa timu ya mtu mmoja. Walisahau kuwa kundi lao dogo la kuipinga timu hiyo lilitosha kuifanya Mtwara kuamini hawakuwa na timu kutokana na matokeo ya uwanjani. Kwa hivi ilikuwa kila siku ikicheza wao walisema “Ndanda hakuna timu. Itashuka tu Daraja.” Walisahau kuwa kila wao walipoomba dua kwa Mungu aishushie maafa timu hiyo, wapo wengi wengine walioiombea mema timu hiyo. Kwa nini wasifungwe?

Wakati ule ilikuwa ngumu sana kwa watu kunielewa nilipoandika kuwa Mtwara tunaihitaji zaidi Ndanda F.C. Wapo ambao walidiriki kusema kwa wazi kabisa kuwa hakuna aliyeihitaji timu hiyo. Hawa ndiyo wanafiki wenyewe – wanafiki ambao wameshafungwa 3-0 na marafiki wa Ndanda.

Nadhani itoshe kuwa kilichotokea kwa Ndanda FC msimu uliopita kuwa funzo kubwa sana kwa Mkoa wa Mtwara – mkoa ambao una historia kubwa sana katika soka la Tanzania. Uvumilivu uliofanywa na Viongozi, wachezaji na mashabiki wa Ndanda ni wa hali ya juu ambao unapaswa kupongezwa kwa nguvu zote.

Bado naamini na nasisitiza kuwa Mtwara tungali tunaihitaji Ndanda FC kuliko Ndanda FC inavyoihitaji Mtwara. Kwa namna yoyote iwayo huu ndiyo wakati pekee wa kuonesha kuwa umoja upo miongoni mwa wanamichezo wa Mtwara – unafiki hauna tija.


Hawawezi kujionesha sasa kwamba wao ndiyo walikuwa mstari wa mbele kuiombea mabaya Ndanda FC lakini wanajulikana. Wakati huu watafurahi na Marafiki halisi wa Ndanda kwa sababu lengo lao limeshindikana. Wanaumia na wataumia zaidi kuiona Ndanda ikiendelea kufanya vizuri miaka mingine ijayo.

No comments :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. The Chief - All Rights Reserved.